18 Oktoba 2026 - 11:45
Wanaharakati Nchini Denmark Waandamana Kupinga Matamshi ya Chuki Dhidi ya Waislamu Yanayoenezwa na Wafuasi wa Mrengo wa Kulia Uliokithiri

Wanaharakati wanaopinga ubaguzi wa rangi mjini Copenhagen wamepinga madai ya mrengo wa kulia uliokithiri kwamba unapambana na Unazi na Uislamu wa kisiasa. Wanaharakati hao walishiriki katika mkusanyiko wa maandamano ya kupinga sera ya kuwafukuza wahamiaji. Kwa mujibu wa mmoja wa waandaaji, kauli hizo haziwezi kuficha chuki dhidi ya Waislamu, ambayo hujitokeza hasa kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– kundi la mashirika yanayopinga ubaguzi wa rangi na wanaharakati wa kiraia mjini Copenhagen, mji mkuu wa Denmark, jana Jumamosi lilikusanyika kupinga maandamano ya mrengo wa kulia uliokithiri yaliyolenga kuunga mkono sera ya “kuwarejesha wahamiaji” au kuwafukuza nchini humo.

Kaulimbiu kuu ya mkusanyiko huo ilikuwa “Hapana kwa Kuwarejesha Wahamiaji.” Waandaaji walisema kuwa kubadilisha kaulimbiu za mrengo wa kulia uliokithiri na kutumia misamiati kama “kupambana na Unazi na Uislamu wa kisiasa” hakuwezi kuficha misingi ya kiitikadi ya vuguvugu hilo na msimamo wake wa kupinga Uislamu.

Lene Junker, mmoja wa wanachama wa mpango wa pamoja dhidi ya ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa aina nyingine, aliikosoa mikondo ya mrengo wa kulia uliokithiri, akisema kuwa makundi hayo yanajaribu kujificha nyuma ya picha za bendera ya Denmark zilizotengenezwa kwa kutumia akili bandia (AI).

Alisisitiza: “Bendera nyingi za Denmark haziwezi kuficha chuki ambayo wafuasi wao wanaielekeza dhidi ya Waislamu, hasa kupitia mitandao ya kijamii.”

Junker pia alipinga madai yanayowalaumu Waislamu kwa matatizo ya kiuchumi na kushuka kwa kiwango cha ustawi wa jamii. Alieleza kuwa kupanda kwa gharama za maisha na kudhoofika kwa huduma za ustawi wa jamii kunatokana na utendaji wa wanasiasa na waajiri wanaoweka shinikizo kwa mishahara na masharti ya kazi.

Mkusanyiko huo ulianza saa 13:00 siku ya Jumamosi katika uwanja wa Halmtorvet, eneo la Vesterbro, mjini Copenhagen. Miongoni mwa waliozungumza katika mkutano huo walikuwa John Ekebjærg, mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi cha 3F Copenhagen, na Sama Ben Haddou, katibu mkuu wa shirika la Mino Denmark.

Waandaaji walisema kuwa lengo la maandamano hayo lilikuwa kupinga kuhalalishwa kwa sera zinazowalenga wahamiaji na kutetea usalama pamoja na haki za wananchi wote.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha